0
MANCHESTER, ENGLAND
JOSE MOURINHO (pichani chini) ameshapata nguvu ya kuweka mambo sawa baada ya Manchester United kuichapa Leicester City mabao 4-1 Old Trafford Jumamosi mchana na sasa amefanya kikao cha dharura na kumpiga biti nahodha wake, Wayne Rooney.
Mourinho alikuwa katika presha ya hali ya juu baada ya United kuchapwa mechi tatu mfululizo, lakini baada ya kumuweka Rooney benchi katika pambano la Leicester amepata nguvu ya kufanya naye mazungumzo ya moyoni na kumuonya jambo.
Kocha huyo Mreno amemwambia Rooney kwamba analazimika kwanza kurudisha fomu yake kabla ya kufungua mdomo wake kulalamikia viwango vya wachezaji wengine katika timu hiyo akiwa kama nahodha baada ya kucheza ovyo siku za karibuni.

Inadaiwa kuwa Rooney alitoa maneno makali wakati wa mapumziko wa pambano kati ya Manchester United na watani zao Manchester City lililopigwa wiki mbili zilizopita ambapo timu hiyo ilikuwa imechapwa mabao 2-0 hadi kufikia wakati wa mapumziko.
Na sasa imebainika kuwa Mourinho alimuita Rooney katika ofisi yake iliyopo uwanja wa mazoezi wa United, Carrington na kumwambia kuwa amepoteza haki ya kuwalaumu wengine mpaka yeye mwenyewe atakaporudisha kiwango chake.
Rooney pia ameambiwa kuwa atalazimika kupigania nafasi yake baada ya wachezaji waliopewa nafasi yake Jumamosi kuonyesha uwezo mzuri kiasi cha mashabiki na wachambuzi wengi kuhoji kama mchezaji huyo ndiye anayeirudisha nyuma timu hiyo pindi anapoanza mechi.

Rooney
Rooney alipumzishwa katika pambano la kwanza la Europa la United dhidi ya Fayenoord jijini Rotterdam hivi karibuni, lakini alipopewa nafasi katika pambano la Watford alionyesha kiwango kibovu huku United ikichapwa mabao 3-1.

Rooney na Mourinho
Alicheza tena katika pambano la Kombe la Ligi dhidi ya Northampton Jumanne iliyopita lakini hakuweza kuthibitisha makali yake huku United ikishinda kwa mabao 4-1 dhidi ya vibonde hao. Na sasa nafasi yake iko hatarini Old Trafford.
Mourinho alidai kwamba alimuacha Rooney katika pambano dhidi ya Leicester City kwa sababu alihitaji wachezaji wenye damu inayochemka zaidi, Marcus Rashford, 18, na Jesse Lingard, 23 kwa ajili ya kumchezesha mshambuliaji mkongwe, Zlatan Ibrahimovich.

Mourinho, Rooney mazoezini.
Huku Juan Mata akichezeshwa namba 10 ambayo imekuwa ikichezwa na Rooney katika siku za karibuni, United ilirudi katika ubora wake katika pambano hilo ambalo hadi mapumziko walikuwa wanaongoza kwa mabao hayo manne kwa mshangao wa mashabiki wengi wa soka duniani walioamini kuwa mechi hiyo ingekuwa ngumu kwa United.

Rooney anatazamiwa kurudi uwanjani katika pambano la Europa dhidi ya Zorya Luhansk, lakini kuna uwezekano mkubwa asianzishwe tena na Mourinho katika pambano la Ligi dhidi ya Stoke City ugenini Jumapili.

Post a Comment

 
Top