0


MANCHESTER, ENGLAND
 NI siku ya hukumu mwanzo mwisho Manchester derby huko Old Trafford
BATO la Old Trafford. Nakwambia mtoto hatumwi dukani, hii ni shughuli ya wakubwa tu. Manchester United na Manchester City. Jose Mourinho na Pep Guardiola. Wa kwanza na wa tatu kwenye msimamo. Ni bato kweli kweli.
Hii ni bato ya Manchester derby. Itapigwa mchana kweupe pale Old Trafford. Kuna vita kubwa ya kuitazama njani ya uwanja kwa dakika zote tisini.

Jose Mourinho v Pep Guardiola
Makocha hao wawili kwa muda mrefu wamekuwa wapinzani. Walianza kuonyeshana ubabe kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kabla ya vita yao kuendelea kwenye El Clasico huko Hispania na sasa watachuana kwenye derby ya kihistoria England, Man United na Man City kwa mara ya kwanza baada ya kujiunga na timu hizo msimu huu.
Makocha hao kabla ya leo, wamekutana mara 16 kwenye michuano tofauti, wakiwa na timu tofauti. Mourinho amemvaa Guardiola akiwa na Chelsea, Inter Milan na Real Madrid, wakati Guardiola alimvaa Mourinho akiwa na Barcelona na Bayern Munich. Vita ya leo itakuwa ya kuonyeshana ubabe nane Mfalme wa Jiji la Manchester.

David De Gea v Claudio Bravo
Hakuna ubishi, Guardiola atampa mechi yake ya kwanza kipa wake mpya Claudio Bravo na mechi hiyo ni mtihani mzito kwake kuhakikisha kwamba ilikuwa sahihi kwake kwenda kusaini Man City na kumwondoa aliyekuwa kipa wao namba moja, Joe Hart.
David De Gea ni kipa mwenye uzoefu tayari wa Ligi Kuu England na kwa misimu kadhaa amekuwa na mchango mkubwa sana katika kuipa matokeo mazuri Man United. Kama eneo ambalo Mourinho hakupata shida kutafuta mtu mpya ni golini kwa sababu ya uwepo wa De Gea, Mhispaniola aliye kwenye ubora wake.

Zlatan Ibrahimovic v John Stones
Pep Guardiola alitua fungu la maana kumsajili beki wa kati John Stones kutoka Everton akitegemea kupata huduma bora kabisa kutoka kwa Mwingereza huyo. Lakini, kipimo chake cha kwanza kigumu kutambua kama kweli anastaahili kucheza kwenye timu kubwa kama Man City ni leo atakapomkabili straika matata, Zlatan Ibrahimovic.
Fowadi huyo wa zamani PSG hadi sasa ameshatikiza wavu mara tatu kwenye Ligi Kuu England, tena akiwa amefunga kwa mabeki wagumu kama Wes Morgan, Robert Huth, Jose Fonte. Je, Stones atamuweza Ibrahimovic kwa soka lake la kibabe? Hii ni vita tamu.


Paul Pogba v David Silva
Vita kali zaidi kwenye Manchester derby itakuwa kwenye sehemu ya kiungo. Mahali hapa Old Trafford itashuhudia vita ya fundi wa mpira kutoka Hispania, David Silva akionyesha kazi na mchezaji ghali duniani, kiungo wa Kifaransa, Paul Pogba. Pogba atataka kuwaonyesha mashabiki wa Man United kwamba hakufanya makosa kurudi kwenye timu hiyo, tena kwa pesa nyingi, lakini Silva naye akitaka kuonyesha kwamba kuucheza mpira ni kitu rahisi zaidi kwake kukifanya.
Vita ya nyota hao wawili ni kwenye kuchezesha timu zao, upande upi utakuwa na mashambulizi zaidi na kiungo gani atakuwa anatengeneza mashambulizi hayo. Hapa ni patamu pia.

Wayne Rooney v Kevin de Bruyne
Hii ni bato ya Namba 10. Wayne Rooney tangu Manchester United ilipokuwa chini ya kocha Mourinho amekuwa akitumika kwenye Namba 10, akicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati. Kwa mahasimu wao, Man City, tangu Guardiola alipotua hapo, Mbelgiji Kevin De Bruyne amekuwa akitumika kwenye Namba 10. Nyota hao wawili, wote ni mafundi wa kupiga asisti, licha ya kwamba De Bruyne ni mtamu zaidi.
Lakini, katika mechi hiyo ya leo, Rooney atakuwa nyumbani na kitendo cha kuwa nahodha atakuwa kwenye mstari wa mbele vitani kuhakikisha Mourinho atashinda vita yake dhidi ya Guardiola. Licha ya kwamba ni mechi ya nne tu kwenye Ligi Kuu, lakini inabeba pia taswira kamili ya ubingwa wa msimu huu.

Anthony Martial v Raheem Sterling
Tangu kuanza kwa msimu huu, Raheem Sterling amekuwa kwenye ubora wake klabuni Man City na kumfanya kocha Guardiola kumwaanzisha kwenye kikosi chake. Akitarajia kushambulia kupitia upande wa kushoto, Man United wao winga wao wa kushoto atakuwa Anthony Martial. Hii ni vita inayosubiriwa kwa hamu kuona ni winga gani kati ya hao wawili atakuwa msumbufu kwa mabeki watakaomkaba, hususani mabeki wa pembeni.
Martial bado hayupo kwenye ubora wake sana, lakini ataingia kwenye mechi hiyo akiwa na kumbukumbu nzuri ya kufanya kweli kwenye mechi za kimataifa akiwa na Ufaransa, hivyo atataka kuhamishia makali ya huko uwanjani Old Trafford.

Eric Bailly v Nolito
Pep Guardiola atakosa huduma ya straika asilia katika mchezo huo wa Manchester derby na hapo anaweza kumtumia Nolito kama Namba 9 feki. Hii ni staili ambayo Guardiola amekuwa akiitumia sana akiwa amewahi kufanya hivyo kwa Lionel Messi alipokuwa Barcelona na Mario Gotze alipokuwa Bayern Munich, huko mchezo wa leo, Nolito anaweza kuanzishwa kama straika.
Lakini, fowadi huyo wa zamani wa Celta Vigo hii leo hapo Old Trafford atakumbana na Eric Bailly, beki wa kati shupavu ambaye aliwahi kukutana naye pia kwenye La Liga, wakati alipokuwa akiipiga Villarreal kabla ya kutua Man United. Bailly tangu kuanza kwa msimu umekuwa kwenye ubora mzuri na jambo hilo limemfanya Mourinho asihangaike kutafuta beki mwingine wa kati baada ya kuona kwamba kombinesheni yake na Daley Blind imekuwa tamu.

Marcus Rashford v Kelechi Iheanacho
Rashford na Iheanacho ni makinda bora kabisa kwenye klabu hizo kwa sasa. Makocha wao wanaweza kuwapa nafasi katika mechi hiyo ya Manchester derby ili waonyeshe makali yao. Rashford si mgeni wa mechi hiyo, ameshawahi kucheza na kufunga pia. Hivi karibuni, makinda hao wote walichezea timu zao za taifa, wakati Iheanacho akiwalaza Tanzania kwenye kuwania kufuzu Afcon 2017 alipokuwa na Nigeria, Rashford alipiga 'hat-trick' alipokuwa na timu ya taifa ya vijana ya England na kumfanya kocha wa timu ya wakubwa, Sam Allardyce kusema kwamba atamrudisha kwenye kikosi cha kwanza cha wakubwa.
Kwenye timu zao, Iheanacho ameanzishwa mara 12 tu, wakati Rashford ameanzishwa mara 18, lakini Iheanacho ameasisti mara tano katika dakika 1291 alizocheza kikosi Man City, wakati Rashford ameasisti mara mbili katika dakika 1452. Iheanacho ana miaka 19, Rashford miaka 18.

Post a Comment

 
Top