LONDON,
ENGLAND
KITENDO
cha Manchester City kumteua kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola
kinamkutanisha kocha huyo na staa wake wa zamani, Yaya Toure ambaye inasemekana
walitofautiana wakati akiwa Barcelona na akamruhusu kuondoka klabuni hapo
kwenda City mwaka 2010.
Hii si mara ya kwanza kwa kitendo kama hicho
kutokea.
Wayne
Rooney vs David Moyes Wawili hawa walikuwa na historia hii. Rooney aliibukia
katika mikono ya Moyes wakati wakiwa Everton. Baadaye Rooney akapakaza katika
kitabu chake kwamba Moyes alikuwa amelazimisha auzwe kwenda Manchester United
kwa dau la Pauni 27 milioni mwaka 2004.
Moyes
akamshtaki Rooney na akashinda kesi ya kupakaziwa na Rooney mnamo mwaka 2007.
Rooney alilazimishwa kumuomba msamaha Moyes na pia kumlipa fidia ya Pauni
150,000.
Wakati
Sir Alex Ferguson alipoachia ukocha Old Trafford, Moyes alipewa kibarua hicho
na kujikuta akikutana tena na ‘Mbaya’ wake, Rooney.
Hata
hivyo, waliua bifu lao na kuthibitisha kwamba limekufa Moyes alimteua Rooney
kuwa nahodha wake.
Jose
Mourinho vs Cesc Fabregas
Kuna kocha mwenye historia ya kukorofishana na
wachezaji wa timu pinzani zaidi ya Mourinho? Bifu kubwa la Mourinho na Fabregas
lilitokana na upinzani mkubwa uliokuwa unaendelea kati ya Barcelona na Real
Madrid wakati huo, Cesc akiwa mchezaji wa Barcelona huku Mourinho akiwa kocha
wa Madrid. Fabregas alikuwa anaongoza vijembe kwa Mourinho wakati bifu likiwa
limepamba moto.
Wakati
Carlo Ancelotti alipotua Real Madrid mara baada ya Mourinho kuondoka Fabregas
alisika akisema: “Kwa sasa hatutakuwa na kocha ambaye anakasirika pindi
mchezaji wa Real Madrid anapoongea na Barcelona.
”
Fabregas alimpiga kijembe Mourinho ambaye alikuwa akikasirika wakati wachezaji
wa Madrid walipokuwa wanaongea na wale wa Barcelona.
Miezi
michache baadaye Fabregas alikuwa akisaini kuichezea Chelsea kwa dau la Pauni
27 milioni huku akidai kuwa sababu kubwa ya kusaini Chelsea ni kwamba Mourinho
alikuwa bonge la kocha.
Kevin Keegan vs Michael Owen
Wawili hawa
waliwahi kukutana katika kikosi cha timu ya taifa ya England.
Owen
alidai kwamba Keegan alikuwa anamuonea kwa kumfanya kisingizio pindi timu hiyo
ilipokuwa inafanya vibaya. “Nadhani nilikuwa naonewa. Kulikuwa na presha kubwa
kwake na alikuwa anahitaji mtu wa kumtoa kafara. Nilianza kutompenda. Sio kama
mtu tu bali kama kocha,” alisema Owen mwaka 2005.
Owen
hakufikiria kama siku moja angecheza tena chini ya Keegan hata hivyo, ilitokea
tena wakati alipokwenda Newcastle United Januari 2008.
Na
siku ambapo Keegan alifukuzwa, Owen alikaririwa akidai kwamba alikuwa na huzuni
sana.
“Kilikuwa
kipindi bora cha maisha yangu ya soka Newcastle. Kila mtu alipenda kucheza
chini yake. Ilikuwa ni fahari kucheza chini yake. Nilifurahia kipindi cha
maisha yangu ya soka pale kuliko kipindi chochote nikiwa na Newcastle,”
alikaririwa Owen Juni 2013.
Jose
Mourinho vs Samuel Eto'o
Kila
mtu anakumbuka jinsi staa huyu wa Cameroon alivyotangaza wazi kwamba asingeweza
kuichezea Chelsea kamwe. Ilikuwa mwaka 2005 wakati timu yake ya zamani
Barcelona ilipopambana na Chelsea katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya
ambapo Mourinho alianzisha vurugu nyingi uwanjani kiasi kwamba mwamuzi wa
pambano hilo, Anders Frisk wa Sweden baadaye aliamua kustaafu soka.
“Kamwe
siwezi kusaini timu inayofundishwa na Mourinho. Aliharibu mambo kabisa katika
mechi mbili baina yetu.
“Nasisitiza,
kocha wa Barca, Frank Rijkaard ni kocha bora licha ya mataji ambayo Mourinho
ameshinda,” alisema Eto’o Machi 2005.
Miaka
minne baadaye Eto’o alikula matapishi yake wakati alipokwenda Inter Milan kisha
Mourinho akahamia klabuni hapo. Baada ya kutwaa taji la Ulaya pamoja alijikuta
akisema “Kabla sijaja Inter Milan, hatukujuana vizuri, kwa hiyo uhusiano wetu
ulikuwa wa ovyo. “Niliwahi hata kusema kuwa nisingeweza kuchezea timu ambayo
Mourinho anafundisha. Lakini Mungu ndiye ajuaye. Alitaka kunionyesha kuwa
nilikosea kusema hivyo na leo Jose ni rafiki yangu,” alisema Eto’o, Septemba
2013.
Yossi
Benayoun vs Rafa Benitez
Moja kati ya sababu ni kwa nini Yossi Benayoun aliamua
kwenda Chelsea ilitokana na kumkimbia Rafa Benitez akiwa Liverpool. Hakujua
kama siku moja Chelsea ingemteua Benitez kuwa kocha wa muda.
Wakati
anahama alisikika akisema “Kila mtu ananiuliza sababu za kuondoka Liverpool.
kuna sababu moja tu, Rafa Benitez. Kama ningecheza vizuri asingenisifia.
Nilipofunga mabao nilitegemea kuwa katika kikosi ambacho kingeanza wiki ijayo.
“Hauwezi
kumtendea mchezaji hivyo na utegemee awe na furaha. Benitez alijaribu kuniua
kama alivyofanya kwa Riera. Chelsea ilitoa ofa na dili lilishakamilika kabla
Benitez hajaondoka,” alisema Benayouna Julai 2010.
Baada
ya Benitez kutua na kumkuta Benayoun Chelsea alijaribu kusahau maneno ya staa
huyo na kumuingiza katika kikosi chake cha kwanza huku akisema “Benayoun ni
sehemu ya timu na anafanya mazoezi na timu. Yossi anaweza kucheza pembeni na
najua akili yake ya soka. Hapana shaka anaweza kutupa kitu.”
Cristiano
Ronaldo vs Jose Mourinho
Kuna bifu baina ya Wareno hawa wawili na halikuanzia
Hispania.
Lilianzia
England wakati Mourinho akiwa kocha wa Chelsea na Ronaldo akiwa staa wa
Manchester United.
Mourinho alimshutumu Ronaldo kuwa alikuwa hana
elimu, hajapevuka kiakili, na mengineyo ya kashfa. Ilikuwa ni baada ya pambano
lao ambalo Mourinho aliishutumu Manchester United kuwa ilikuwa inapewa penalti
nyingi zisizo sahihi huku Ronaldo akijibu mapigo kuwa Mourinho alikuwa ni mgumu
kukiri kushindwa kwake.
Miaka
kadhaa baadaye walikutana Santiago Bernabeu kama mchezaji na kocha wake na
uhusiano wao haukuwa mzuri huku Ronaldo akilalamika kwamba klabu hiyo ilikuwa
inakabiliwa na ‘hali mbaya ya hewa’.
El
Hadji Diouf vs Neil Warnock
Ilikuwa ni katika pambano la FA kati ya QPR na
Blackburn Rovers Januari 2011 huku Diouf akiwa mchezaji wa Blackburn na Warnock
akiwa kocha wa QPR. Diouf alimshambulia kwa matusi mchezaji wake, Jamie Mackie
ambaye alikuwa amelala chini ya majeraha akiamini kuwa alikuwa anadanganya.
Ni
kweli Mackie alikuwa ameumia na kitendo hicho cha Diouf kiliwakera wengi
uwanjani hasa Warnock ambaye mwisho wa mechi alisema: “Nadhani (Diouf) ni mtu
asiye na hadhi kabisa. Natumaini aende nje ya nchi kwa sababu sitammiss
kumtazama wakati akicheza. Ni mtu mjinga kabisa,” alisema Warnock, Januari
2011.
Septemba
2012, Warnock aligeuka kuwa mnafiki wa hali ya juu kabisa baada ya kuamua
kumnunua mshambuliaji huyo wakati akiwa kocha wa Leeds Unted.
Alijitetea
akisema :“Hakuna aliyewahi kumsema vibaya zaidi yangu, lakini nilikutana naye
katika kipindi cha majira ya joto, baada ya kumwambia ukweli wangu
tulimalizana,” alisema Warnock Septemba 2012.
Post a Comment