LIVERPOOL, ENGLAND
JURGEN KLOPP ametupwa nje katika michuano ya Kombe la Ligi maarufu
kama Carabao na Leicster City na kuzusha hali ya sintofahamu ndani ya kikosi
chake cha Liverpool.
Siku chache zilizopita kikosi hicho kimetoka kufungwa mabao 5-0 na
Manchester City kisha ikalazimishwa sare na Burnley na juzi usiku ikichezea
kichapo cha mabao 2-0 na kutupwa nje mapema kabisa katika michuano hiyo.
Mabao ya Shinji Okazaki na Islam Slimani yalitosha kuivusha
Leicester City kwenye hatua nyingi na kumuacha Klopp akifura kwa hasira huku
akieelekeza lawama kwa safu yake ya ulinzi.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Klopp alisema amechoshwa na
safu yake ya ulinzi na kwamba, wamefungwa mabao mepesi sana bila washambuliaji
wa Leicester kuvuja jasho.
“Inaumiza mno kuruhusu mabao kama yale. Leicester imepambana
uwanjani lakini imetufunga mabao mepesi sana. Imefunga kiulaini sana kiasi
cha kunifanya kuumwa,” alisema Klopp, ambaye kwenye mchezo huo alifanya
mabadiliko ambayo mpaka sasa yamekuwa gumzo kwa mashabiki.
Katika mchezo huo, Klopp alimtoa kiungo wake wa nguvu Philippe
Coutinho baada ya dakika 45 za kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na kinda Ben
Woodburn, ambaye hakuweza kufurukuta na kuwafanya Liverpool kupoteana.
“Tuna timu nzuri na kikosi cha kazi, lakini inashangaza kuona
tumeondolewa kwenye mashindano wakati tulipaswa kusonga mbele kwa hatua
nyingine. Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza lakini tumeshindwa kufunga mabao
na hilo linatokea kwenye soka,” alisema.
Hata hivyo, Klopp alitetea uamuzi wake wa kumtoa Coutinho
akisema ilikuwa ni mipango aliyoweka kabla hata ya kuanza kwa mchezo huo. Klopp
alisema kwenye mchezo huo alipanga kumchezesha kiungo huyo wa Kibrazili kwa
dakika 45 tu ili kumfanya kuwa fiti zaidi.
Jumamosi, Liverpool itaraejea tena kwenye dimba la King Power
kuikabili Leicester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England.
Post a Comment