0


                       PARIS, UFARANSA
DAN ALVES amemfanyia kitu mbaya Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola baada ya kukamilisha usajili wake Paris Saint Germain (PSG).
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya beki huyo wa zamani wa Juventus kuchana na miamba hiyo ya Turin, mwezi uliopita.
Beki huyo wa kulia wa kimataifa Brazil mwenye umri wa miaka 34- kwa kiasi kikubwa alikuwa akitarajiwa kuungana tena na kocha wake wa zamani wa Barcelona, Guardiola kikosini Manchester City.
Habari za kujiunga na PSG badala ya Man City zimewashtua wadau wengi zilipoanza kuripotiwa mapema wiki hii.
Jumamosi iliyopita, Alves alikuwa akifunga ndoa na mpenzi wake katika Fukwe za Ibiza kule Hispania na Manchester City ilikuwa ina uhakika kuwa mara baada ya tukio hilo, angesaini mkataba uliokuwa mezani ili atue Ligi Kuu England.
 PSG imetoa ofa zaidi ya Manchester City ya Pauni 230,000 kwa wiki kwa beki huyo wa zamani wa Sevilla kwa mkataba wa miaka miwili.

Dani Alves akikabidhiwa jezi
Inadaiwa pia kuna uwezekano mkubwa kuwa mke wa Alves amependelea zaidi kuishi Paris, jiji linalojulikana kwa matanuzi makubwa na limekuwa kichocheo kwa wanasoka wanaotakiwa na PSG.

....akikaribishwa PSG
Hilo linakuwa pigo kubwa kwa Guardiola dhidi ya Alves ambaye alitwaa mataji 23 akiwa na Barcelona, matatu yakiwa ya Ulaya na sita ya La Liga huku akiwa mmoja kati ya wachezaji wa mwanzoni kununuliwa na Guardiola pale Nou Camp akitokea Sevilla mwaka 2008 na hivi karibuni aliwahi kumwelezea Guardiola kama kocha mwenye akili nyingi.

... akiwa na skafu ya PSG
Kutokana na hatua hiyo ya Alves, City sasa inalazimika kuhamishia mipango yake na nguvu zote kwa beki wa kulia wa Tottenham, Kyle Walker, ambaye Spurs ipo tayari kuachana naye kama City itafika dau la Pauni 50 milioni. Akizungumza baada ya kumwaga wino PSG, Alves alisema: "Kuna mradi wa kuvutia hapa Paris, nina marafiki hapa na mimi ni mtu ninayependa changamoto. Kama nimewaumiza Guardiola na Manchester City, ninawaomba msamaha. Lakini nimekuja hapa kutwaa ubingwa."
"Nilikuwa na presha ya kushinda Ligi ya Mabingwa kwa miaka mitatu, nimekuja kuleta uzoefu wangu hapa. Rais (wa PSG) ana ushawishi mkubwa, nataka kuandika historia, tunaweza kuandika pamoja. Kazi ambayo klabu imefanya kwa miaka kadhaa inatia moyo. Ni timu yenye nia."
Guardiola anasaka mabeki wanne wa pembeni baada ya kuachana na Gael Clichy, Bacary Sagna na Pablo Zabaleta na mpaka sasa bado hajafanikiwa kumshawishi beki yeyote kutua kikosini hapo.
Kocha huyo wa zamani wa Bayern pia inadaiwa kuwa anamsaka beki wa kushoto wa Monaco, Benjamin Mendy, ambaye pia atamgharimu pesa nyingi wakati huu Monaco ikidhamiria kupata zaidi ya Pauni 40 milioni kwa staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa.
Mastaa wengine ambao sasa wanaweza kuangaliwa na Guardiola ni pamoja na beki wa kulia wa PSG, Serge Aurier, ambaye nafasi yake itakuwa shakani baada ya kuwasili kwa Alves huku kukiwa na malalamiko mengi ya kinidhamu kwa staa huyo wa Ivory Coast.

                   ...PSG kuna ushawishi mkubwa hapa
Wengine ni pamoja na beki wa kulia wa Benfica, Nelson Semedo, aliyekuwa anaelekea Barcelona lakini mpaka sasa dili lake linasemekana halijakamilika. Vilevile kuna beki wa kulia wa Bayer Leverkusen, Benjamin Henrichs na beki wa kulia wa Arsenal, Hector Bellerin.
Guardiola pia anajiandaa kupambana na pigo jingine baada ya Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, kutangaza wazi kwamba hadhamirii kuachana na staa wake, Alexis Sanchez ambaye inadaiwa kuwa Manchester City imekuwa ikimnyemelea kwa nguvu zote katika dirisha hili huku akiwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja tu Emirates.Inadaiwa Alves atapata mara mbili PSG zaidi ya kile ambacho Man City ilichopanga kumpatia.

...Alves amemuomba radhi Guardiola
Hata hivyo, uamuzi wake labda umechangiwa na uwezekano mkubwa wa kushinda medali akiwa na PSG.
Dan Alves ambaye ameshinda mataji akiwa na Barcelona na Juventus, sasa anaangalia uwezekano wa kuongeza medali nyingine kwa kutwaa taji la Ufaransa wakati PSG ikipambana kurudisha taji la Ligue 1 kutoka kwa Monaco.

Post a Comment

 
Top