NA ABEID
POLO
HUU
ni msimu wa pili. Pep Guardiola akiwa na Manchester City na Jose Mourinho akiwa
na Manchester United. Huo ni mlingano wa kwanza baina ya makocha hao wawili
wenye upinzani mkali kwenye kazi yao. Kwa msimu huu, kila mmoja ameiongoza timu
yake kwenye mechi sita, tano kwenye Ligi Kuu England na moja kwenye Ligi ya
Mabingwa Ulaya. Kila mmoja ameshinda mechi tano kati ya hizo na kutoka sare
moja. Mlingano mwingine huu baina ya makocha hao. Achana na hilo. Kitu kinachonivutia
ni kile kilichoibuka katika Ligi Kuu England. Wameufanya msimu huu kuwa wa timu
za kutoka Manchester. Manchester City na Manchester United ndizo timu
zinazokabana kileleni, pointi tatu zaidi ya mabingwa hawa watetezi, Chelsea kutoka
London.
Lakini, kwa hii kasi iliyoanza nayo Manchester City na Manchester
United, inafanya kuwapo kwa dalili za wazi kabisa mbio za ubingwa wa msimu huu kwenye ligi hiyo,
inaweza kuwa ya farasi wawili. Manchester United na Manchester City au Mourinho
na Guardiola. Kila mmoja amecheza mechi tano, amekusanya pointi 13. Kila mmoja
amefunga mabao 16 na amefungwa mabao mawili. Wanalingana kila kitu. Kila mmoja
alijaribu kutengeneza timu yake kupambana kwenye ligi kuhakikisha kuna kitu
kinavunwa katika msimu huu.
Walau
kwa Mourinho, msimu uliopita aliokoteza mataji matatu; Ngao ya Jamii, Kombe la
Ligi na Europa League. Lakini, kwa Guardiola upande wake, ulikuwa mtupu.
Hakukuwa na taji lolote na hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kumaliza msimu
mikono mitupu. Haikuwa hivyo tangu huko alikotokea, Barcelona na Bayern Munich.
Msimu
huu anapambana na hali yake yasitokee ya msimu uliopita. Wiki hii wawili hao
walihamishia vita yao kwenye Kombe la Ligi. Manchester City ilicheza na West
Brom ugenini na Manchester United ikiwa nyumbani ilicheza na Burton Albion.
Hadithi imeendelea kuwa ileile, kila mmoja amepata ushindi wa mabao.
Manchester
United imeshinda mabao 4-1 na Manchester City imeshinda 2-1.
Kwa
kasi ya kufunga zaidi ya mabao 19 au 20 katika mechi sita za Ligi Kuu si jambo dogo.
Hiki ndicho walichofanya makocha hao wawili katika vikosi vyao. Jose ana mabao
19 na Pep ana mabao 20. Kila mmoja amejipanga vyema na silaha zake. Hiki ndicho
kitu kinachofanya ligi ya msimu huu kuwa na mvuto. Ni wazi kabisa, Arsene
Wenger, Antonio Conte, Mauricio Pochettino na Jurgen Klopp watakuwa wanakuna
vichwa juu ya wapinzani wao wawili. Klopp amekumbana na mmoja wao, Pep na
amekutana na alichokutana nacho. Sasa ni dhahiri, wengine waliobaki watakuwa na
wasiwasi mkubwa watakapokutana na mmoja wa makocha hao wawili.
Ni
suala la kufikirisha pia, wawili hao watakapokutana kwa mara ya kwanza msimu
huu. Nini kitatokea. Lakini, kubwa ni kasi hii walioanza nayo, Jose na Pep,
wametupa kitu cha kufuatilia kwa karibu!...
Post a Comment