LONDON, ENGLAND
MAMBO yanazidi
kupamba moto. Bifu la Chelsea na staa wake, Diego Costa linataka kwenda mbali
zaidi kwa sasa. Inaaminika Chelsea inafikiria kumshtaki Costa mahakamani na
kumdai kiasi cha Pauni 50 milioni kama ataendelea kugoma kurudi klabuni.
Chelsea inaamini
staa huyo wa kimataifa wa Hispania, mzaliwa wa Brazil anavunja masharti ya
mkataba wake na klabu hiyo ambayo inamlipa mshahara wa Pauni 185,000 kwa wiki
huku mkataba huo ukiwa umebakiza miaka miwili.
Costa ametajwa
katika kikosi cha wachezaji 25 wa Chelsea ambao, watashiriki katika Ligi Kuu ya
msimu huu, lakini jina lake halipo katika orodha ya wachezaji watakaoiwakilisha
klabu hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Inadaiwa kuwa mwenyewe
kwa sasa anazungumza na wanasheria wake.
Uhusiano wa Costa
na Kocha wa Chelsea, Antonio Conte umekuwa mchungu zaidi baada ya staa huyo
kushindwa kufanikiwa azma yake ya kurudi katika klabu yake ya zamani, Atletico
Madrid siku moja baada ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho la Hispania.
Chelsea
imesisitiza Costa bado anaendelea kuwa mchezaji wake na ni lazima arudi
kuendelea kuutumikia mkataba wake. Costa anadai uhusiano wake na Chelsea
ulikufa pale tu Kocha Conte alipomtumia meseji kwamba, hakuwa katika mipango
yake tena.
Costa amekubali kufanya mazungumzo na Chelsea.
Kwa miezi miwili
sasa Costa amejichimbia katika Jiji la Rio de Janeiro, Brazil huku akiendeleza
vita ya maneno na Conte, lakini sasa suala lao linaweza kwenda pabaya zaidi
wakati huu Chelsea ikifikiria kumshitaki.
Chelsea
inajulikana kwa masuala ya mahakamani na mara ya mwisho ililazimika kumlipa
daktari wa timu yao, Eva Carneiro kiasi cha Pauni 5 milioni baada ya
kubwatukiana na kocha wa Chelsea wa wakati huo, Jose Mourinho.
Hata hivyo,
inadaiwa kuwa Costa amekubali kukaa meza moja na Chelsea na kufanya mazungumzo
ya Amani.
Wakati huo huo,
klabu ya Atletico Madrid imemuomba Costa arudi katika mazoezi ya kikosi cha
Chelsea kwa ajili ya kumaliza suala hilo na hivyo itamchukua kwa amani kutoka
kwa mabingwa hao wa England.
Atletico ndio
klabu pekee ambayo inataka kumchukua Costa kwa sasa baada ya kumuuza kwenda
Chelsea kwa dau la Pauni 32 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto
mwaka 2014.
Tangu hapo Costa
na Atletico wamekuwa katika uhusiano mzuri. Endapo Costa atarudi mazoezini
Chelsea kuna uwezekano mkubwa akajikuta akiishia katika kikosi cha wachezaji wa
akiba, lakini bado atakuwa akijiweka katika nafasi nzuri kujiunga na Atletico dirisha
la Januari.
Chelsea imepitia
katika kipindi cha ovyo cha dirisha la uhamisho licha ya kufanikiwa kuwanasa
mastaa Alvaro Morata kutoka Real Madrid, Tiemoue Bakayoko kutoka Monaco, Danny
Drinkwater kutoka Leicester City, Antonio Rudiger kutoka Roma na Willy
Caballero iliyemnasa bure kutoka Manchester City.
Mastaa watatu
waligoma kujiunga na timu hiyo katika dirisha hili. Romelu Lukaku, Alex
Oxlade-Chamberlain, na Ross Barkley wote waliitosa Chelsea na sasa presha
imepelekwa kwa wakurugenzi wawili wa Chelsea, Marina Granovskaia na Michael
Emenalo.
Costa akiwa na hasimu wake, Conte enzi zao.
Conte, ambaye
amekuwa hana mamlaka ya kisheria katika mazungumzo na wachezaji wapya klabuni,
ameonekana kukerewa na suala la wachezaji hao kukataa kuhamia Chelsea huku
tajiri wa timu Abramovich akitaka maelezo ya kina kutaka kujua kwanini mastaa
hao waliitosa Chelsea.
Post a Comment